Fathers of the Clan

Fathers of the Clan

CHAPAULINGE FAMILY

In God We Trust and In Jesus We Make Through to Heaven. Amen

Sunday, 18 May 2014

JE, WAJUA HISTORIA FUPI YA UKOO WA CHAPAULINGE? HEBU SOMA HAPA CHINI


Mzee Akimu Chapaulinge Mataje 

Mzee Jimmy Mrisho Mataje

MKOA WA MBEYA

WILAYA YA CHUNYA

MJI MDOGO WA MAKONGOLOSI

Ramani ya Mbeya na Chunya ikionesha kijiji cha Makongolosi na eneo la asili.
IMEANDALIWA NA: MAWAZO AKIMU CHAPAULINGE MATAJE

TOLEO LA KWANZA
 
CHAPISHO LA MWAKA – 2013

CHAPISHO HILI LIMEANDALIWA NA:

·         MAWAZO AKIMU CHAPAULINGE MATAJE

SIMULIZI NA MAELEZO TOKA KWA:

·         BABA AKIMU CHAPAULINGE MATAJE

·         BABA JIMMY MRISHO MATAJE

·         BABA HASSAN CHAPAULINGE MATAJE

·         BABA ANDERSON MRISHO CHAPAULINGE

·         KAKA PAUL MOSES CHAPAULINGE

·         AKINA MAMA WA MZEE AKIMU

·         NDUGU WA UKOO WA CHAPAULINGE

ONYO

Maelezo, michoro na picha zote katika historia hii ni mali ya ukoo wa Chapaulinge kwa makusudi na malengo ya ukoo. Hairuhusiwi kwa mtu yeyote kunakili, kuhamisha au kutumia kwa namna yoyote ile maelezo na michoro au picha zilizopo katika historia hii bila idhini ya ukoo wa Chapaulinge.

© Copyright – 2013

Ukoo wa Chapaulinge
Mnara wa uhuru kama unavyoonekana eneo la Mbeya mjini

UTANGULIZI

Historia hii ya ukoo wa Chapaulinge ni hatua ya kwanza katika kuiweka kwa maandishi asili ya ukoo wetu. Hakujawahi kuwa na historia yoyote ya ukoo katika maandishi na wazazi wetu ndio wanazeeka hivyo ni jukumu la sisi tuliosoma kuiweka historia yetu katika maandishi ili watoto na wajukuu zetu kama Mungu akitujalia uhai waweze kuisoma na kuelewa asili yao. Historia hii itaendelea kuboreshwa kulingana na vyanzo mbalimbali vya habari na matukio mengine ambayo yataongezeka au kuboresha baadhi ya maelezo katika nyaraka hii. Hivyo, waraka huu au historia hii sio mwisho wa kuandika isipokuwa ni mwanzo wa safari ndefu ya kuandika na kuboresha historia ya ukoo wetu wa Chapaulinge.

Kwa namna ya pekee napenda kutoa shukrani kwa Mungu wetu wa Ibrahim, Isaka na Yakobo kwa kunipa uhai na nguvu za kuandika historia hii. Vilevile, natoa shukrani kwa baba Jimmy, Baba Hassan, akina mama wote, kaka Paulo pamoja na ndugu wengine waliofanikisha katika kuandika historia hii iwe kwa kutoa maelezo au kwa kutoa mchango wao namna ya kuandika vizuri historia hii. Siwezi kutaja wote walioshiriki lakini nawashukuru wote waliochangia katika kuboresha kazi hii ya kuandika asili yetu

KIDOKEZO
Historia ya ukoo wa Chapaulinge ni ndefu lakini pia bado ina mapungufu yake hasa asili ya ndani kabisa ya ukoo. Hata hivyo, taarifa muhimu zimepatikana kuhusiana na ukoo wetu ingawa sio za kina sana. Tutajifunza zaidi kuhusu asili ya ukoo wetu hapo chini kwa undani zaidi.

Malengo ya kuandika historia hii ni mengi lakini makubwa ni:-

  1. Kuweka kumbukumbu sahihi na endelevu kuhusu ukoo wetu na vizazi vijavyo
  2. Kujenga utamaduni wa kuandika historia za maisha yetu kwa faida ya watoto wetu na ndugu zetu.
  3. Kuondoa utata kuhusu asili ya ukoo wetu na ndugu zetu ambao kuna hatari ya kupotezena nao baadae.

Kuna faidi nyingi za kuandika historia, baadhi ya hizo ni:-
  1. Kusaidia watoto wetu kujifunza asili ya maisha yao na ndugu zao wengine
  2. Kuweka kumbukumbu sahihi za ukoo wetu ili zisipotee
  3. Kuondoa hatari ya ukoo kutojuana na kufahamiana hapo baadae
  4. Historia inasaidia hata kuondoa migongano ya kuingiliana. Mfano watoto wa baba mmoja au ndugu wa karibu kuona bila kujua asili yao
 
CHANGAMOTO WAKATI WA KUANDIKA HISTORIA
Baadhi ya changamoto wakati wa kuandika historia ni:-

  1. Wazee kusahau baadhi ya mambo kwa sababu ya kutoandika au kutokuwa na kumbukumbu vizuri
  2. Baadhi ya taarifa kutokuwa na uhakika wa usahihi wake
  3. Kukosekana kwa asili ya ndani ya ukoo wetu
  4. Baadhi ya matukio kufichwa au kutosemwa kutokana na sababu za ugomvi au matatizo ya ukoo.
Ukoo huu una tamaduni zinazofanana na koo zingine kwa sababu kabila la Wabungu ni wabantu yaani makabila yanayoongea lugha na mila au tamaduni zinazofanana. Neno utamaduni ni kubwa na pana sana kwa sababu linajumuisha maisha ya watu ya kila siku pamoja na shughuli za kila siku. Baadhi ya tamaduni hizo ni kama zifuatazo:-

  • Ukoo wetu bado una mila na utamaduni wa kurithi pale mtu anapofariki. Hapo zamani ilikuwa mume akifariki, mke anarithiwa na ndugu mwingine kama tutakavyoona katika historia hii hapo chini. Hata hivyo, uamuzi wa kurithi ulibaki kuwa wa mwanamke kwa mtindo wa kubeba kibuyu au chombo chenye pombe na kutembea kwa magoti hadi kwa mtu yule anayetaka kumrithi. Iwapo mke wa marehemu hataki kurithiwa, basi alikuwa anampatia pombe hiyo mtoto wake kama ishara ya kukataa kurithiwa. Utaratibu wa mila hii upo sehemu nyingi sana katika nchi hii. Hata hivyo, mila hii siku hizi imeanza kubadilika kwa sababu hapo zamani mtu akifariki anarithi jina na mke lakini siku hizi urithi unakuwa wa jina tu na majukumu mengine ya kutatua matatizo ya ukoo lakini hauna haki ya kuchukua mali au mke wa marehemu.
  • Pia, hapo zamani mmoja wa wanandugu anapofariki, ndugu wote walikuwa wanakaa bila kuoga kwa muda wa siku tatu na kuendelea mpaka siku ya kuoga maji ambapo msiba unamalizwa kwa wana ndugu wote kukatwa nywele kwa ajili ya matambiko na mambo mengine. Mila hii inaitwa kufagia kikunku – yaani kusafisha nyumba na kumaliza msiba baada ya siku chache toka marehemu alipozikwa. Utamaduni huu bado upo ingawa siku hizi watu wanaoga kila siku wakati wa msiba.
  • Wakati wa msiba hapo zamani na hata sasa kwa baadhi ya maeneo yetu ya ndani kabisa, bado kuna wana ndugu ambao hukata kitambaa ambacho marehemu atazikiwa (sanda) na kujifunga ndugu wote sehemu ya mkokoni au shingoni kwa kipindi hicho cha msiba. Wana ndugu wote ilikuwa ni lazima kujifunga kipande cha sanda ambacho marehemu amezikiwa kama ishara ya kushiriki msiba pamoja nae na pia kwa ajili ya imani za matambiko ya ukoo. Siku ya kumaliza msiba kamba za sanda huondolewa na kupewa wazee kwa jili ya kufanya yanayoendelea.
  • Hapo zamani ilikuwa ni marufuku kwa mtoto au ndugu yeyote kula mazao ya shambani kabla ya baba na mama hawajafanya matambiko. Matambiko yalikuwa ya aina mbili. Kwanza wakati wa kulima (kabla ya kupanda mazao) na pili kabla ya kuvuna. Baba mwenye shamba alikuwa anavuna mahindi kiasi au zao lile alilolima na kufanya matambiko kabla ya watu kuanza kula. Hata hivyo, mila hii siku hizi imepungua sana baada ya watu kugundua hakuna madhara yoyote katika maisha yao. Lakini baadhi ya watu wanadai kuwa mila hii ilikuwa inasaidia kupunguza njaa kwa sababu mahindi yalikuwa yanakaa hadi yanakomaa kabisa na hivyo kipindi cha kula mahindi mabichi kilikuwa kifupi. Hali hiyo ilifanya wazee wetu wavune mahindi makavu ya kutosha tofauti na sasa ambapo shamba linaweza kwisha hata kabla ya mazao hayajakauka shambani.
  • Ukoo wetu hapo zamani ulikuwa unaamini sana katika mizimu au babu zetu waliokufa kama akina Chapaulinge, Mrisho na Mataje. Babu zetu hao waliaminika kuwa na nguvu ya kutusaidia katika matatizo yetu ya kawaida. Mara nyingine baba zetu walikuwa wanaongea na hao babu zetu kupitia Ngoma za asili na nyimbo maalum za kuamsha mizimu. Baba zetu wote walikuwa wamejenga vijumba vidogo kwa ajili ya matambiko kwa hao babu zetu. Kila kijumba kidogo kiliwakilisha mzimu au babu aliyefariki ambaye kwa imani iliaminika bado alikuwa anakaa katika kijumba kile. Katika kijumba hicho wazee wetu waliweka pombe, chakula, nguo, kiti na vitu vingine ambavyo iliaminika mizimu watavitumia. Mila na imani hii hata leo bado ipo na inaendelea kuaminiwa. Baadhi ya ndugu wameanza kuamini katika dini za Kikristo na uislamu. Yesu Kristo ndiyo jibu pekee katika Maisha yetu.
Baadhi ya vijumba ambavyo vinaaminika mizimu ya babu zetu hukaa humu na kufanyiwa matambiko ya kutatua matatizo mbalimbali
 
  • Pia, katika ukoo wetu watu hupenda kufanya kazi kwa kusadiana kwa mtindo unaoitwa “Ndanjira” ambapo mwenye shamba hualika watu au majirani na huandaa chakula na pombe kwa ajili ya watu kuja kulima katika shamba lake. Utamaduni huu unafanyika kwa wale tu ambao ni wanachama katika kusaidiana kulima mashamba. Huu ni utamaduni mzuri ambao hata leo bado upo na umekuwa ukisaidia sana wazee ambao hawana nguvu ya kulima mashamba makubwa.
  • Mwana ndugu anapofariki na msiba kumalizika, hukaa kwa muda Fulani na kurudi tena kumaliza msiba. Watu hukusanyika na kupika pombe ya “Mwengulo”. Mwengulo ni sherehe ya kumaliza msiba ambapo pombe na vyakula hupikwa na wana ndugu wanateua mrithi wa marehemu. Mrithi huyo hairuhusiwi kutoka katika baba mmoja na marehemu ila kutoka kwa baba wadogo au wakubwa au ndugu wengine wa karibu.
  • Hizi ni baadhi tu ya mila na tamaduni zetu na zitaendelea kuborehswa na kuongezwa kadili wana ndugu watakavyochangia.

FAHARI YA KUJIVUNIA
Ni jambo la kujivunia kwamba ukoo wa Chapaulinge umeendelea kuwa mkubwa na wenye heshima kubwa katika wilaya ya Chunya na Mkoa wa Mbeya kwa sehemu. Sisi kama watoto wa uzao ujao tuna kila sababu ya kuenzi mazuri yote yaliyofanywa na wazee wetu lakini pia kufanya marekebisho katika yale yote ambayo yalileta hatari ya kututenganisha.

Sina shaka kuwa historia hii fupi itafungua ukurasa wa watoto wengi kufahamiana hata kwa majina tu na kujua kuwa fulani na fulani ni sehemu ya ukoo. Sisi kama watoto wa Chapaulinge tuna kila sababu ya kujisikia fahari katika ukoo huu pamoja na matatizo mbalimbali kwa sababu hakuna ukoo usio kuwa na matatizo na jambo la muhimu ni namna gani ukoo unatatua hayo matatizo. Ni matarajio yangu kuwa historia hii itasomwa na wana ndugu wote kwa faida ya wote.

Kwa kuwa watoto wengi katika ukoo wa Chapaulinge wameanza kupata elimu na kusambaa, limekuwa jambo la msingi sana kusisitiza umoja na mshikamano katika kuweka sawa mambo mbalimbali.



Ukoo huu wa Chapaulinge kama jinsi wengi walivyozoea kuita una maelezo mengi kama tutakavyoona hapo chini. Kutokana na maelezo ya Baba Jimmy, asili ya ukoo huu wa Chapaulinge ni eneo moja katika kijiji cha Gua linaloitwa Manda chini. Hivyo, sisi kabila letu rasmi ni Wabungu wa eneo la Manda ambako babu zetu walikaa huko. Baadhi ya watu wanaita Manda kama kabila lakini si kabila ila ni eneo ambalo ndiko babu zetu walitokea. Hivyo, ukoo wa Chapaulinge asili yake ni eneo la Manda huko Gua na kabila letu ni wabungu.

MWANZO WA UKOO
Kwa maelezo ya baba Jimmy, wazazi wetu wa kwanza kabisa kwa mujibu wa kumbukumbu ni wawili. Babu wa kwanza alikuwa ni MTWALE na wa pili alikuwa ni MATAJE. Hakuna maelezo yoyote mengine juu ya baba wa akina Mataje na Mtwale. Hivyo, tunaweza kusema kuwa wazazi wetu wa kwanza kabisa ni Mtwale na Mataje ingawa baba yao hajulikani jina lake. Ndugu wengi hawajui kuwa kuna babu mwingine anaitwa MTWALE. Hata hivyo, kuna taarifa kuwa inawezekana jina la Mwanachambo au Kawenga ni baba ya akina Mataje na Mtwale. Pia, inaelezwa kuwa ukoo huu una asili ya Umwene (Ufalme) kutoka kwa babu zetu wa zamani. Kumbukumbu zingine zikipatikana tunaweza kuboresha eneo hili la historia yetu. Kwa sasa inatosha kusema kuwa wazee wa kwanza kabisa katika ukoo ni MTWALE na MATAJE ingawa Mtwale hafahamiki sana kwa ndugu wengi. Nitaeleza hapo chini kwa nini ndugu wengi hawamfahamu Mtwale.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyopo, watu hao wawili yaani Mtwale na Mataje walifanikiwa kupata watoto lakini kwa sababu mbalimbali za kutoelewana kati ya upande wa Mataje na Mtwale, hakuna maelezo ya kina kuhusu uzao upande wa Mtwale. Hapa ndipo penye kazi kubwa ya kujua kwa kina kwa sababu baba zetu wanakiri kuwa kuna ukoo wa akina Mtwale lakini ni miaka mingi sana hawana mawasiliano nao na hivyo ni kama tayari undugu ulivunjika kati ya watoto wa Mataje na Mtwale. Ukoo huu wa akina Mtwale inasemekana uko maeneo ya Bondeni na baadhi ya majina ya akina Mwile na Mtwale yapo katika maeneo hayo.

Kama tulivyoona hapo juu, baba ambaye wazee wetu hawawezi kukumbuka jina lake alifanikiwa kupata watoto wawili (2) ambao ni Mataje na Mtwale (hawa ni babu wa baba zetu sisi).

Hivyo, kwa upande wa Mtwale hakuna historia ya wazi juu ya watoto waliozaliwa ingawa wapo na yawezekana hata leo wapo maeneo ya Bondeni na sehemu zingine. Inasemekana kuwa moja ya ndugu zetu katika upande wa akina Mtwale ni Mwanachambo aliyekuwa baba yetu na alikaa kwa muda mrefu na mzee Akimu. Huyu Mwanachambo inasemekana alitokea ukoo wa Mtwale.

Pia, kuna shangazi yetu mwingine kwa upande wa akina Mtwale aliyekuwa akiishi maeneo ya Sumbawanga. Shangazi yetu huyu inasemekana aliwahi kuja Makongolosi kwa mzee Akimu kipindi cha nyuma lakini taarifa zake hazipo tena. Watu hawa wawili (shangazi na Mwanachambo) inaonyesha kuwa kuna ndugu katika upande wa akina Mtwale. Hata hivyo, inasemekana matatizo ya ukoo hasa urithi wa mali ulileta mvutano na ugomvi kiasi cha kukatika mawasiliano. Mgogoro huo wa urithi wa mali/ndugu ulisababisha ndugu wa pande mbili kufarakana na kusambaratika. Hivyo, tutaangalia upande mmoja tu wa Mataje ambako sisi tumetokea.

Mataje alizaliwa pamoja na Mtwale maeneo ya Manda chini huko Gua, katika mwambao wa ziwa Rukwa, kata ya Gua wilaya ya Chunya, mkoa wa Mbeya. Wote wawili yaani Mtwale na Mataje walikulia huko Manda chini. Baada ya kuwa watu wazima wote wawili walikwenda kuoa maeneo ya Bondeni katika sehemu iliyoitwa Mwanda (maeneo ya Tete). Baada ya kuoa walikaa huko na kuanzisha maisha yao huko Bondeni.

Mataje alifanikiwa kuoa huko Bondeni na kupata watoto wa nne (4) kama wafuatao:-

  1. Chapaulinge (mtoto wa kiume)
  2. Mrisho (mtoto wa kiume)
  3. Msia (mtoto wa kike)
  4. Junjulu (mtoto wa kike)

MAISHA YA KAWAIDA YA MATAJE
Mataje alizaliwa huko maeneo ya Gua – Manda katika mwambao wa ziwa Rukwa. Mataje alikuwa mkulima na kidogo mfugaji kwa kiasi Fulani. Pia, aliishi kwa kutegemea kazi ya uvuvi ingawa haikua ya kipato sana kwa wakati huo. Maelezo ya maisha ya kawaida ya Mataje hayawezi kuwa marefu kwa sababu hakuna kumbukumbu sahihi za kutosha kuelezea maisha yake kwa undani zaidi.

Baada ya kufanikiwa kupata hao watoto 4, Mataje alifia Bondeni na kuzikwa huko. Hivyo uzao wa Mataje ukaishia hapo.


UZAO ULIOFUATA BAADA YA MATAJE
Ifuatayo ni historia au uzao uliofuata baada ya Mataje kwa maana ya wajukuu wa Mataje (yaani watoto wa akina Chapaulinge, Mrisho, Msia na Junjulu).

Chapaulinge alifanikiwa kumuoa Mbaji katika ukoo wa akina Nenje wenyeji wa Lupa Tingatinga na kupata watoto watano (5). Na baada ya kufariki Mrisho, Chapaulinge alirithi Nsendo Nankombe (mke wa babu Mrisho) na kupata mtoto mwingine wa kike aliyeitwa Msia au Agness (mama Nsendo). Hivyo, Chapaulinge alikuwa na watoto sita (6) ambao ni:-
  1. Mwile (mtoto wa kiume)
  2. Mitemo (mtoto wa kike)
  3. Akimu (mtoto wa kiume) huyu alikuwa pacha (Kulwa au Mpaasi kwa jina la asili)
  4. Jonas (mtoto wa kiume) huyu alikuwa pacha (Doto au Nyuuma kwa jina la asili)
  5. Hassani (mtoto wa kiume) huyu pia aliitwa Zyola (Yaani mtoto anayefuata baada ya mapacha huitwa Zyola)
  6. Agness (Msia au mama Nsendo) alizaliwa baada ya Chapaulinge kurithi mke wa mdogo wake (Mrisho)
Kwa mujibu wa maelezo ya baba Jimmy, Chapaulinge alihama kutoka Bondeni Mwanda hadi Kisungu na kuanzisha maisha mapya huko. Katika watoto wa Mataje hapo juu, ni Chapaulinge peke yake aliyehamia Kisungu. Chapaulinge alizaliwa huko Bondeni eneo la Mwanda pamoja na ndugu wengine. Maisha ya kawaida ya Chapaulinge yalikuwa ya ukulima kwa wakati huo. Inasemekana kuwa Chapaulinge alikuwa mkali sana lakini alipendana sana na Mrisho. Ilikuwa haiwezekani mmoja augue na kupitisha siku au siku chache bila kuonana na mwenzake. Wakati mwingine iliwalazimu kutembea hata usiku ili kuonana kunapotokea shida kati yao. Baba Jimmy anasimulia kuwa hao wawili walisaidiana sana na walikuwa kitu kimoja ingawa hawakukaa pamoja. Babu yetu Chapaulinge aliishi Kisungu na alifia Kisungu na hata leo kuna eneo linalotunzwa kwa ajili ya kaburi lake. Hivyo, maisha ya baba zetu kwa ujumla walilelewa huko Kisungu.

WATOTO WA MRISHO
Baada ya Mrisho kufikia umri wa kuoa alikwenda kumuoa Nsendo Nankombe katika ukoo wa akina Mwavilondo hukohuko Bondeni maeneo ya Mwanda. Mrisho alifanikiwa kupata watoto watatu (3) ambao ni:-

  1. Moses
  2. Jimmy
  3. Anderson
Kwa bahati mbaya, Mrisho alifariki mapema sana na hivyo kumuacha bibi (Nankombe) akiwa bado mzima. Na kwa mujibu wa mila za wakati huo, bibi Nankombe alirithiwa na babu Chapaulinge wa Kisungu. Na hivyo kufanikiwa kupata mtoto mwingine wa kike aliyeitwa Agness (kwa jina la asili ni Msia au alifahamika sana kwa jina la mama Nsendo).

Mrisho pia alizaliwa huko Bondeni eneo la Mwanda pamoja na akina Chapaulinge. Kama yalivyo maelezo ya Chapaulinge, alipendana sana na Chapaulinge ambaye alikuwa mtu na kaka yake. Mrisho aliishi Bondeni na kuolea huko na hata maisha yake yalikuwa huko hadi kufariki. Alikuwa na maisha ya ukulima kama walivyo babu wengine katika historia hii.

Baada ya kufariki alizikwa hukohuko Bondeni na bibi yetu aliyeitwa Nsendo Nankombe alikwenda Kisungu na kurithiwa na babu Chapaulinge. Baada ya urithi huo, akazaliwa Agnes (Msia au mama Nsendo) ambaye alikuwa shangazi yetu pamoja na Mitemo.

Msia alikuwa mtoto wa babu Mataje lakini hakubahatika kuwa na watoto wakakua, wote walizaliwa na kufariki. Hivyo, alifariki akiwa hana watoto.

Msia alizaliwa Bondeni pia pamoja na kaka zake akina Mrisho. Kwa maelezo ya baba Jimmy, Msia alibahatika kupata watoto lakini wote walifariki kabla hawajafikisha umri mkubwa. Hivyo, hakuna historia wala uzao wake uliobaki baada ya yeye kufariki. Yeye pia alifia Bondeni na kuzikwa huko pamoja na Mataje


Junjulu alikuwa pia mtoto wa babu Mataje lakini hakubahatika kupata watoto kabisa katika maisha yake.
Junjulu alizaliwa Bondeni pamoja na akina Chapaulinge. Huyu hakuwa na watoto kabisa na hivyo historia yake ni fupi sana. Hata hili jina lake halitumiki sana katika watoto wengine. Nadhani ni moja kati ya majina ambayo yamejificha sana na hayatumiwi na ndugu wengi. Huyu pia alifia Bondeni na kuzikwa huko pamoja na ndugu wengine.
Hivyo tunaweza kusema kuwa katika watoto 4 ambao Mataje alifanikiwa kuwapata, ni watoto wawili (2) tu walioweza kuendeleza ukoo ambao ni Mrisho na Chapaulinge.  Mrisho na Chapaulinge ndio waliondeleza ukoo kwa maana ya kuoa na kufanikiwa kupata watoto ambao nao walizaa. Hawa wawili tunaweza kusema ndio kiunganishi cha ukoo mzima kwa maana ya kuwa ndio walioweza kukaa vizuri na hata kuwaunganisha watoto ambao ndio baba zetu na babu wa watoto wetu kwa sasa. Tunahitaji kuwakumbuka wazee wetu waliobaki kwa sababu ndio msingi wa ukoo wetu.

Hii ni historia fupi sana ya ukoo wa Chapaulinge. Nimeandika maelezo mengi sana kuhusu uko wetu na historia ya kila mwana Ndugu. Kwa sasa siwezi kuiweka hapa mpaka nitakapopata uhakika wa baadhi ya taarifa. Pia, hata historia hii iliyowekwa hapa bado inahitaji marekebisho kutoka kwa wadau mbalimbali wa ukoo. Mnakaribishwa kutoa michango ya kuboresha historia yetu. Mungu awabariki sana. Ameni.

No comments:

Post a Comment