Mzee Akimu Chapaulinge Mataje
|
Mzee Jimmy Mrisho Mataje |
MKOA WA MBEYA
WILAYA YA CHUNYA
MJI MDOGO WA MAKONGOLOSI
|
Ramani ya Mbeya na Chunya ikionesha kijiji cha Makongolosi na eneo la asili. |
IMEANDALIWA
NA: MAWAZO AKIMU
CHAPAULINGE MATAJE
TOLEO LA KWANZA
CHAPISHO LA MWAKA – 2013
CHAPISHO
HILI LIMEANDALIWA NA:
·
MAWAZO
AKIMU CHAPAULINGE MATAJE
SIMULIZI
NA MAELEZO TOKA KWA:
·
BABA
AKIMU CHAPAULINGE MATAJE
·
BABA
JIMMY MRISHO MATAJE
·
BABA
HASSAN CHAPAULINGE MATAJE
·
BABA
ANDERSON MRISHO CHAPAULINGE
·
KAKA
PAUL MOSES CHAPAULINGE
·
AKINA
MAMA WA MZEE AKIMU
·
NDUGU
WA UKOO WA CHAPAULINGE
ONYO
Maelezo, michoro na picha zote katika
historia hii ni mali ya ukoo wa Chapaulinge kwa makusudi na malengo ya ukoo.
Hairuhusiwi kwa mtu yeyote kunakili, kuhamisha au kutumia kwa namna yoyote ile
maelezo na michoro au picha zilizopo katika historia hii bila idhini ya ukoo wa
Chapaulinge.
©
Copyright – 2013
Ukoo
wa Chapaulinge
|
Mnara wa uhuru kama unavyoonekana eneo la Mbeya mjini |
UTANGULIZI
Historia hii ya ukoo wa Chapaulinge ni hatua ya kwanza katika
kuiweka kwa maandishi asili ya ukoo wetu. Hakujawahi kuwa na historia yoyote ya
ukoo katika maandishi na wazazi wetu ndio wanazeeka hivyo ni jukumu la sisi
tuliosoma kuiweka historia yetu katika maandishi ili watoto na wajukuu zetu
kama Mungu akitujalia uhai waweze kuisoma na kuelewa asili yao. Historia hii itaendelea kuboreshwa
kulingana na vyanzo mbalimbali vya habari na matukio mengine ambayo
yataongezeka au kuboresha baadhi ya maelezo katika nyaraka hii. Hivyo, waraka
huu au historia hii sio mwisho wa kuandika isipokuwa ni mwanzo wa safari ndefu
ya kuandika na kuboresha historia ya ukoo wetu wa Chapaulinge.
Kwa namna ya pekee napenda kutoa
shukrani kwa Mungu wetu wa Ibrahim, Isaka na Yakobo kwa kunipa uhai na nguvu za
kuandika historia hii. Vilevile, natoa shukrani kwa baba Jimmy, Baba Hassan,
akina mama wote, kaka Paulo pamoja na ndugu wengine waliofanikisha katika
kuandika historia hii iwe kwa kutoa maelezo au kwa kutoa mchango wao namna ya
kuandika vizuri historia hii. Siwezi kutaja wote walioshiriki lakini
nawashukuru wote waliochangia katika kuboresha kazi hii ya kuandika asili yetu
KIDOKEZO
Historia ya ukoo wa Chapaulinge ni
ndefu lakini pia bado ina mapungufu yake hasa asili ya ndani kabisa ya ukoo.
Hata hivyo, taarifa muhimu zimepatikana kuhusiana na ukoo wetu ingawa sio za
kina sana. Tutajifunza
zaidi kuhusu asili ya ukoo wetu hapo chini kwa undani zaidi.
Malengo ya kuandika historia hii ni
mengi lakini makubwa ni:-
- Kuweka
kumbukumbu sahihi na endelevu kuhusu ukoo wetu na vizazi vijavyo
- Kujenga
utamaduni wa kuandika historia za maisha yetu kwa faida ya watoto wetu na
ndugu zetu.
- Kuondoa
utata kuhusu asili ya ukoo wetu na ndugu zetu ambao kuna hatari ya
kupotezena nao baadae.
Kuna faidi nyingi za kuandika
historia, baadhi ya hizo ni:-
- Kusaidia
watoto wetu kujifunza asili ya maisha yao na ndugu zao wengine
- Kuweka
kumbukumbu sahihi za ukoo wetu ili zisipotee
- Kuondoa hatari ya ukoo kutojuana na kufahamiana hapo baadae
- Historia
inasaidia hata kuondoa migongano ya kuingiliana. Mfano watoto wa baba
mmoja au ndugu wa karibu kuona bila kujua asili yao
CHANGAMOTO WAKATI WA KUANDIKA HISTORIA
Baadhi ya changamoto wakati wa
kuandika historia ni:-
- Wazee
kusahau baadhi ya mambo kwa sababu ya kutoandika au kutokuwa na kumbukumbu
vizuri
- Baadhi
ya taarifa kutokuwa na uhakika wa usahihi wake
- Kukosekana
kwa asili ya ndani ya ukoo wetu
- Baadhi
ya matukio kufichwa au kutosemwa kutokana na sababu za ugomvi au matatizo
ya ukoo.
Ukoo huu una
tamaduni zinazofanana na koo zingine kwa sababu kabila la Wabungu ni wabantu
yaani makabila yanayoongea lugha na mila au tamaduni zinazofanana. Neno
utamaduni ni kubwa na pana sana kwa sababu linajumuisha maisha ya watu ya kila
siku pamoja na shughuli za kila siku. Baadhi
ya tamaduni hizo ni kama zifuatazo:-
- Ukoo
wetu bado una mila na utamaduni wa kurithi pale mtu anapofariki. Hapo
zamani ilikuwa mume akifariki, mke anarithiwa na ndugu mwingine kama tutakavyoona katika historia hii hapo chini.
Hata hivyo, uamuzi wa kurithi ulibaki kuwa wa mwanamke kwa mtindo wa
kubeba kibuyu au chombo chenye pombe na kutembea kwa magoti hadi kwa mtu
yule anayetaka kumrithi. Iwapo mke wa marehemu hataki kurithiwa, basi
alikuwa anampatia pombe hiyo mtoto wake kama
ishara ya kukataa kurithiwa. Utaratibu wa mila hii upo sehemu nyingi sana katika nchi hii.
Hata hivyo, mila hii siku hizi imeanza kubadilika kwa sababu hapo zamani
mtu akifariki anarithi jina na mke lakini siku hizi urithi unakuwa wa jina
tu na majukumu mengine ya kutatua matatizo ya ukoo lakini hauna haki ya
kuchukua mali
au mke wa marehemu.
- Pia,
hapo zamani mmoja wa wanandugu anapofariki, ndugu wote walikuwa wanakaa
bila kuoga kwa muda wa siku tatu na kuendelea mpaka siku ya kuoga maji
ambapo msiba unamalizwa kwa wana ndugu wote kukatwa nywele kwa ajili ya
matambiko na mambo mengine. Mila hii inaitwa kufagia kikunku – yaani
kusafisha nyumba na kumaliza msiba baada ya siku chache toka marehemu
alipozikwa. Utamaduni huu bado upo ingawa siku hizi watu wanaoga kila siku
wakati wa msiba.
- Wakati
wa msiba hapo zamani na hata sasa kwa baadhi ya maeneo yetu ya ndani
kabisa, bado kuna wana ndugu ambao hukata kitambaa ambacho marehemu
atazikiwa (sanda) na kujifunga ndugu wote sehemu ya mkokoni au shingoni
kwa kipindi hicho cha msiba. Wana ndugu wote ilikuwa ni lazima kujifunga
kipande cha sanda ambacho marehemu amezikiwa kama
ishara ya kushiriki msiba pamoja nae na pia kwa ajili ya imani za
matambiko ya ukoo. Siku ya kumaliza msiba kamba za sanda huondolewa na
kupewa wazee kwa jili ya kufanya yanayoendelea.
- Hapo
zamani ilikuwa ni marufuku kwa mtoto au ndugu yeyote kula mazao ya
shambani kabla ya baba na mama hawajafanya matambiko. Matambiko yalikuwa
ya aina mbili. Kwanza wakati wa kulima
(kabla ya kupanda mazao) na pili kabla ya kuvuna. Baba mwenye shamba
alikuwa anavuna mahindi kiasi au zao lile alilolima na kufanya matambiko kabla
ya watu kuanza kula. Hata hivyo, mila hii siku hizi imepungua sana baada ya watu kugundua hakuna madhara yoyote
katika maisha yao.
Lakini baadhi ya watu wanadai kuwa mila hii ilikuwa inasaidia kupunguza
njaa kwa sababu mahindi yalikuwa yanakaa hadi yanakomaa kabisa na hivyo
kipindi cha kula mahindi mabichi kilikuwa kifupi. Hali hiyo ilifanya wazee
wetu wavune mahindi makavu ya kutosha tofauti na sasa ambapo shamba linaweza
kwisha hata kabla ya mazao hayajakauka shambani.
- Ukoo
wetu hapo zamani ulikuwa unaamini sana
katika mizimu au babu zetu waliokufa kama
akina Chapaulinge, Mrisho na Mataje. Babu zetu hao waliaminika kuwa na
nguvu ya kutusaidia katika matatizo yetu ya kawaida. Mara nyingine baba
zetu walikuwa wanaongea na hao babu zetu kupitia Ngoma za asili na nyimbo
maalum za kuamsha mizimu. Baba zetu wote walikuwa wamejenga vijumba vidogo
kwa ajili ya matambiko kwa hao babu zetu. Kila kijumba kidogo
kiliwakilisha mzimu au babu aliyefariki ambaye kwa imani iliaminika bado
alikuwa anakaa katika kijumba kile. Katika kijumba hicho wazee wetu
waliweka pombe, chakula, nguo, kiti na vitu vingine ambavyo iliaminika
mizimu watavitumia. Mila na imani hii hata leo bado ipo na inaendelea
kuaminiwa. Baadhi ya ndugu wameanza kuamini katika dini za Kikristo na
uislamu. Yesu Kristo ndiyo jibu pekee katika Maisha yetu.
|
Baadhi ya vijumba ambavyo vinaaminika mizimu ya babu zetu hukaa humu na kufanyiwa matambiko ya kutatua matatizo mbalimbali |
- Pia,
katika ukoo wetu watu hupenda kufanya kazi kwa kusadiana kwa mtindo
unaoitwa “Ndanjira” ambapo mwenye shamba hualika watu au majirani na
huandaa chakula na pombe kwa ajili ya watu kuja kulima katika shamba lake.
Utamaduni huu unafanyika kwa wale tu ambao ni wanachama katika kusaidiana
kulima mashamba. Huu ni utamaduni mzuri ambao hata leo bado upo na umekuwa
ukisaidia sana
wazee ambao hawana nguvu ya kulima mashamba makubwa.
- Mwana
ndugu anapofariki na msiba kumalizika, hukaa kwa muda Fulani na kurudi
tena kumaliza msiba. Watu hukusanyika na kupika pombe ya “Mwengulo”.
Mwengulo ni sherehe ya kumaliza msiba ambapo pombe na vyakula hupikwa na
wana ndugu wanateua mrithi wa marehemu. Mrithi huyo hairuhusiwi kutoka
katika baba mmoja na marehemu ila kutoka kwa baba wadogo au wakubwa au
ndugu wengine wa karibu.
- Hizi ni
baadhi tu ya mila na tamaduni zetu na zitaendelea kuborehswa na kuongezwa
kadili wana ndugu watakavyochangia.
FAHARI
YA KUJIVUNIA
Ni jambo la kujivunia kwamba
ukoo wa Chapaulinge umeendelea kuwa mkubwa na wenye heshima kubwa katika wilaya
ya Chunya na Mkoa wa Mbeya kwa sehemu. Sisi kama watoto wa uzao ujao tuna kila
sababu ya kuenzi mazuri yote yaliyofanywa na wazee wetu lakini pia kufanya
marekebisho katika yale yote ambayo yalileta hatari ya kututenganisha.
Sina shaka kuwa historia hii
fupi itafungua ukurasa wa watoto wengi kufahamiana hata kwa majina tu na kujua
kuwa fulani na fulani ni sehemu ya ukoo. Sisi kama watoto wa Chapaulinge tuna
kila sababu ya kujisikia fahari katika ukoo huu pamoja na matatizo mbalimbali
kwa sababu hakuna ukoo usio kuwa na matatizo na jambo la muhimu ni namna gani
ukoo unatatua hayo matatizo. Ni matarajio yangu kuwa historia hii itasomwa na
wana ndugu wote kwa faida ya wote.
Kwa kuwa watoto wengi katika
ukoo wa Chapaulinge wameanza kupata elimu na kusambaa, limekuwa jambo la msingi
sana kusisitiza umoja na mshikamano katika kuweka sawa mambo mbalimbali.
Ukoo huu wa Chapaulinge kama jinsi
wengi walivyozoea kuita una maelezo mengi kama tutakavyoona hapo chini. Kutokana
na maelezo ya Baba Jimmy, asili ya ukoo huu wa Chapaulinge ni eneo moja katika kijiji cha Gua linaloitwa Manda
chini. Hivyo, sisi kabila letu rasmi ni Wabungu wa eneo la Manda ambako babu
zetu walikaa huko. Baadhi ya watu wanaita Manda kama
kabila lakini si kabila ila ni eneo ambalo ndiko babu zetu walitokea. Hivyo,
ukoo wa Chapaulinge asili yake ni eneo la Manda huko Gua na kabila letu ni
wabungu.
MWANZO WA UKOO
Kwa maelezo ya
baba Jimmy, wazazi wetu wa kwanza kabisa kwa mujibu wa kumbukumbu ni wawili. Babu
wa kwanza alikuwa ni MTWALE na wa
pili alikuwa ni MATAJE. Hakuna
maelezo yoyote mengine juu ya baba wa akina Mataje na Mtwale. Hivyo, tunaweza
kusema kuwa wazazi wetu wa kwanza kabisa ni Mtwale na Mataje ingawa baba yao
hajulikani jina lake. Ndugu wengi hawajui kuwa kuna babu mwingine anaitwa MTWALE. Hata hivyo, kuna taarifa kuwa
inawezekana jina la Mwanachambo au Kawenga ni baba ya akina Mataje na Mtwale.
Pia, inaelezwa kuwa ukoo huu una asili ya Umwene (Ufalme) kutoka kwa babu zetu
wa zamani. Kumbukumbu zingine zikipatikana tunaweza kuboresha eneo hili la
historia yetu. Kwa sasa inatosha kusema kuwa wazee wa kwanza kabisa katika ukoo
ni MTWALE na MATAJE ingawa Mtwale
hafahamiki sana kwa ndugu wengi. Nitaeleza hapo chini kwa nini ndugu wengi
hawamfahamu Mtwale.
Kwa mujibu wa
maelezo yaliyopo, watu hao wawili yaani Mtwale na Mataje walifanikiwa kupata
watoto lakini kwa sababu mbalimbali za kutoelewana kati ya upande wa Mataje na
Mtwale, hakuna maelezo ya kina kuhusu uzao upande wa Mtwale. Hapa ndipo penye
kazi kubwa ya kujua kwa kina kwa sababu baba zetu wanakiri kuwa kuna ukoo wa
akina Mtwale lakini ni miaka mingi sana hawana mawasiliano nao na hivyo ni kama
tayari undugu ulivunjika kati ya watoto wa Mataje na Mtwale. Ukoo huu wa akina
Mtwale inasemekana uko maeneo ya Bondeni na baadhi ya majina ya akina Mwile na Mtwale
yapo katika maeneo hayo.
Kama tulivyoona
hapo juu, baba ambaye wazee wetu hawawezi kukumbuka jina lake alifanikiwa
kupata watoto wawili (2) ambao ni Mataje na Mtwale (hawa ni babu wa baba zetu
sisi).
Hivyo, kwa upande
wa Mtwale hakuna historia ya wazi juu ya watoto waliozaliwa ingawa wapo na yawezekana
hata leo wapo maeneo ya Bondeni na sehemu zingine. Inasemekana kuwa moja ya
ndugu zetu katika upande wa akina Mtwale ni Mwanachambo aliyekuwa baba yetu na
alikaa kwa muda mrefu na mzee Akimu. Huyu Mwanachambo inasemekana alitokea ukoo
wa Mtwale.
Pia, kuna
shangazi yetu mwingine kwa upande wa akina Mtwale aliyekuwa akiishi maeneo ya
Sumbawanga. Shangazi yetu huyu inasemekana aliwahi kuja Makongolosi kwa mzee
Akimu kipindi cha nyuma lakini taarifa zake hazipo tena. Watu hawa wawili
(shangazi na Mwanachambo) inaonyesha kuwa kuna ndugu katika upande wa akina
Mtwale. Hata hivyo, inasemekana matatizo ya ukoo hasa urithi wa mali ulileta
mvutano na ugomvi kiasi cha kukatika mawasiliano. Mgogoro huo wa urithi wa
mali/ndugu ulisababisha ndugu wa pande mbili kufarakana na kusambaratika.
Hivyo, tutaangalia upande mmoja tu wa Mataje ambako sisi tumetokea.
Mataje alizaliwa
pamoja na Mtwale maeneo ya Manda chini huko Gua, katika mwambao wa ziwa Rukwa,
kata ya Gua wilaya ya Chunya, mkoa wa Mbeya. Wote wawili yaani Mtwale na Mataje walikulia huko Manda
chini. Baada ya kuwa watu wazima wote wawili walikwenda kuoa maeneo ya Bondeni
katika sehemu iliyoitwa Mwanda (maeneo ya Tete). Baada ya kuoa walikaa huko na
kuanzisha maisha yao
huko Bondeni.
Mataje alifanikiwa kuoa huko Bondeni
na kupata watoto wa nne (4) kama wafuatao:-
- Chapaulinge
(mtoto wa kiume)
- Mrisho
(mtoto wa kiume)
- Msia
(mtoto wa kike)
- Junjulu
(mtoto wa kike)
MAISHA YA KAWAIDA YA MATAJE
Mataje alizaliwa huko maeneo ya Gua –
Manda katika mwambao wa ziwa Rukwa. Mataje alikuwa mkulima na kidogo mfugaji
kwa kiasi Fulani. Pia, aliishi kwa kutegemea kazi ya uvuvi ingawa haikua ya
kipato sana kwa
wakati huo. Maelezo ya maisha ya kawaida ya Mataje hayawezi kuwa marefu kwa
sababu hakuna kumbukumbu sahihi za kutosha kuelezea maisha yake kwa undani
zaidi.
Baada ya kufanikiwa kupata hao watoto
4, Mataje alifia Bondeni na kuzikwa huko. Hivyo uzao wa Mataje ukaishia hapo.
UZAO
ULIOFUATA BAADA YA MATAJE
Ifuatayo ni historia au uzao uliofuata
baada ya Mataje kwa maana ya wajukuu wa Mataje (yaani watoto wa akina
Chapaulinge, Mrisho, Msia na Junjulu).
Chapaulinge alifanikiwa kumuoa Mbaji
katika ukoo wa akina Nenje wenyeji wa Lupa Tingatinga na kupata watoto watano
(5). Na baada ya kufariki Mrisho, Chapaulinge alirithi Nsendo Nankombe (mke wa
babu Mrisho) na kupata mtoto mwingine wa kike aliyeitwa Msia au Agness (mama
Nsendo). Hivyo, Chapaulinge alikuwa na watoto sita (6) ambao ni:-
- Mwile
(mtoto wa kiume)
- Mitemo
(mtoto wa kike)
- Akimu
(mtoto wa kiume) huyu alikuwa pacha (Kulwa au Mpaasi kwa jina la asili)
- Jonas (mtoto wa kiume) huyu alikuwa pacha (Doto au
Nyuuma kwa jina la asili)
- Hassani (mtoto wa kiume) huyu pia aliitwa Zyola (Yaani
mtoto anayefuata baada ya mapacha huitwa Zyola)
- Agness (Msia au mama Nsendo) alizaliwa baada ya
Chapaulinge kurithi mke wa mdogo wake (Mrisho)
Kwa mujibu wa
maelezo ya baba Jimmy, Chapaulinge alihama kutoka Bondeni Mwanda hadi Kisungu
na kuanzisha maisha mapya huko. Katika
watoto wa Mataje hapo juu, ni Chapaulinge peke yake aliyehamia Kisungu. Chapaulinge
alizaliwa huko Bondeni eneo la Mwanda pamoja na ndugu wengine. Maisha ya
kawaida ya Chapaulinge yalikuwa ya ukulima kwa wakati huo. Inasemekana kuwa
Chapaulinge alikuwa mkali sana lakini alipendana
sana na Mrisho.
Ilikuwa haiwezekani mmoja augue na kupitisha siku au siku chache bila kuonana
na mwenzake. Wakati mwingine iliwalazimu kutembea hata usiku ili kuonana kunapotokea
shida kati yao.
Baba Jimmy anasimulia kuwa hao wawili walisaidiana sana na walikuwa kitu kimoja
ingawa hawakukaa pamoja. Babu yetu Chapaulinge aliishi Kisungu na alifia
Kisungu na hata leo kuna eneo linalotunzwa kwa ajili ya kaburi lake. Hivyo, maisha
ya baba zetu kwa ujumla walilelewa huko Kisungu.
WATOTO WA MRISHO
Baada ya Mrisho kufikia umri wa kuoa
alikwenda kumuoa Nsendo Nankombe katika ukoo wa akina Mwavilondo hukohuko
Bondeni maeneo ya Mwanda. Mrisho alifanikiwa kupata watoto watatu (3) ambao
ni:-
- Moses
- Jimmy
- Anderson
Kwa bahati mbaya, Mrisho alifariki
mapema sana na
hivyo kumuacha bibi (Nankombe) akiwa bado mzima. Na kwa mujibu wa mila za
wakati huo, bibi Nankombe alirithiwa na babu Chapaulinge wa Kisungu. Na hivyo
kufanikiwa kupata mtoto mwingine wa kike aliyeitwa Agness (kwa jina la asili ni
Msia au alifahamika sana
kwa jina la mama Nsendo).
Mrisho pia alizaliwa huko Bondeni eneo
la Mwanda pamoja na akina Chapaulinge. Kama yalivyo maelezo ya Chapaulinge,
alipendana sana
na Chapaulinge ambaye alikuwa mtu na kaka yake. Mrisho aliishi Bondeni na
kuolea huko na hata maisha yake yalikuwa huko hadi kufariki. Alikuwa na maisha
ya ukulima kama walivyo babu wengine katika
historia hii.
Baada ya kufariki alizikwa hukohuko
Bondeni na bibi yetu aliyeitwa Nsendo Nankombe alikwenda Kisungu na kurithiwa
na babu Chapaulinge. Baada ya urithi huo, akazaliwa Agnes (Msia au mama Nsendo)
ambaye alikuwa shangazi yetu pamoja na Mitemo.
Msia alikuwa mtoto wa babu Mataje
lakini hakubahatika kuwa na watoto wakakua, wote walizaliwa na kufariki. Hivyo,
alifariki akiwa hana watoto.
Msia alizaliwa Bondeni pia pamoja na
kaka zake akina Mrisho. Kwa maelezo ya baba Jimmy, Msia alibahatika kupata
watoto lakini wote walifariki kabla hawajafikisha umri mkubwa. Hivyo, hakuna
historia wala uzao wake uliobaki baada ya yeye kufariki. Yeye pia alifia
Bondeni na kuzikwa huko pamoja na Mataje
Junjulu alikuwa pia mtoto wa babu
Mataje lakini hakubahatika kupata watoto kabisa katika maisha yake.
Junjulu alizaliwa Bondeni pamoja na
akina Chapaulinge. Huyu hakuwa na watoto kabisa na hivyo historia yake ni fupi sana. Hata hili jina lake halitumiki
sana katika watoto
wengine. Nadhani ni moja kati ya majina ambayo yamejificha sana na hayatumiwi na ndugu wengi. Huyu pia
alifia Bondeni na kuzikwa huko pamoja na ndugu wengine.
Hivyo tunaweza kusema kuwa katika
watoto 4 ambao Mataje alifanikiwa kuwapata, ni watoto wawili (2) tu walioweza
kuendeleza ukoo ambao ni Mrisho na Chapaulinge. Mrisho na Chapaulinge ndio waliondeleza ukoo
kwa maana ya kuoa na kufanikiwa kupata watoto ambao nao walizaa. Hawa wawili
tunaweza kusema ndio kiunganishi cha ukoo mzima kwa maana ya kuwa ndio
walioweza kukaa vizuri na hata kuwaunganisha watoto ambao ndio baba zetu na
babu wa watoto wetu kwa sasa. Tunahitaji kuwakumbuka wazee wetu waliobaki kwa
sababu ndio msingi wa ukoo wetu.
Hii ni historia fupi sana ya ukoo wa Chapaulinge. Nimeandika maelezo mengi sana kuhusu uko wetu na historia ya kila mwana Ndugu. Kwa sasa siwezi kuiweka hapa mpaka nitakapopata uhakika wa baadhi ya taarifa. Pia, hata historia hii iliyowekwa hapa bado inahitaji marekebisho kutoka kwa wadau mbalimbali wa ukoo. Mnakaribishwa kutoa michango ya kuboresha historia yetu. Mungu awabariki sana. Ameni.